MASOMO YA MISA, JUMATANO YA JUMA LA NNE LA KWARESIMA, MACHI 18, 2026

MASOMO YA MISA, JUMATANO YA JUMA LA NNE LA KWARESIMA, MACHI 18, 2026

Mar 18, 2026

 JUMATANO YA JUMA LA NNE LA KWARESIMA,

SOMO I


ISAYA 49:8—15

Nimekufanya uwe agano kwa watu, ili niinue tena nchi.Bwana Mungu asema hivi: “Wakati wa kufaa nimekujibu; na katika siku ya wokovu nimekuletea shime. Nitakuhifadhi na kukufanya uwe agano kwa watu. Nitaiinua tena nchi na kuwapa tena urithi uliokuwa umeachwa. Nitawaambia wafungwa: Tokeni nje! Na walio gizani: Jionyesheni! Katika njia zote watajilisha, juu ya milima yote ya majabali watapata malisho. Hawataona njaa tena wala kiu; hawatapigwa na upepo wa hari wala jua; kwa kuwa Yule aliyewahurumia atawaongoza, na kuwapeleka kwenye mabubujiko ya maji. Nitageuza milima yote kuwa njia, na barabara zitakuzwa. Wengine watatoka mbali: wengine upande wa kaskazini na magharibi, wengine nchi ya Sinimu.” Shangilieni, enyi mbingu; ewe nchi piga vigelegele; nanyi milima, pazeni sauti ya kuimba. Kwa kuwa Bwana amewafariji watu wake, na kuwaonea huruma wenye kuteswa. Sioni alisema, “Bwana ameniacha, Bwana wangu amenisahau.” Je, mwanamke aweza kumsahau mtoto wake, aweza kumsahau mzao wa tumbo lake asimhurumie? Hata kama yeye angemsahau, lakini mimi siyakusahau wewe hata kidogo.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.

ZABURI YA KUITIKIZANA


ZABURI 145:8—9, 13cd—14, 17—18 (K. 8a)

K. Bwana ni mwema na mwingi wa huruma.

Bwana ni mwenye huruma na mpole,

sio mwepesi wa hasira, ni mwingi wa huruma.

Bwana ni mwema kwa wote,

na huruma yake i juu ya viumbe vyake vyote. K.

Bwana ni mwaminifu kwa ahadi zake,

na mwenye upendo kwa kazi zake zote.

Bwana huwategemeza wote wanaoanguka,

Huwainua wote waliogandamizwa. K.

Bwana ni mwenye haki katika njia zake zote,

na mwema kwa kazi zake zote.

Bwana u karibu na wote wakuitao,

wote wakuitao kwa uaminifu. K.

 INJILI


YOHANE 5:17—30

Kama Baba anavyowafufua wafu na kuwapa uzima, vivyo hivyo naye Mwana anawapa uzima wale awapendao.

 Somo katika Injili takatifu ilivyoandikwa na Yohane

Wakati ule: Yesu aliwajibu Wayahudi akisema, “Baba yangu anaendelea na kazi yake, name ninafanya vivyo hivyo..” Hapo Wayahudi walizidi kutafuta nafasi ya kumwua, sio kwa sababu alivunja Sabato tu, ila pia kwa sababu alimwita Mungu baba yakena hivyo kujifanya sawa na Mungu. Yesu akajibu akawaambia, “Amin, amin nawaambieni, Mwana hawezi kufanya kitu ila anachomwona Baba akifanya; afanyavyo yeye, Mwana pia anafanya. Kwa maana Baba ampenda Mwana, na anamwonyesha yale atendayo; juu ya hayo, atamwonyesha matendo makubwa zaidi; hata ninyi mtastaajabu. Maana kama Baba anavyofufua wafu na kuwapa uzima, vivyo hivyo na Mwana anawapa uzima awapendao. Aidha Baba hamhukumu mtu, ila amempa Mwana hukumu yote, ili wote wamheshimu Mwana, kama wanavyomheshimu Baba. Asiyemheshimu Mwana hamheshimu Baba aliyemtuma. Amin, amin, nawaambieni, saa inakuja, na ndio sasa, wafu watakaposikia sauti ya Mwana wa Mungu, nao watakaoisikia watakuwa wazima. Maana kama Baba anao uzima ndani yake, hivyo alimpa Mwana pia kuwa na uzima ndani yake. Akampa mamlaka ya kufanya hukumu, kwa sababu ni Mwana wa Mtu. Msistaajabie hayo, kwa maana saa inakuja watakaposikia sauti yake wote waliomo makaburini, na watatoka, wale waliotenda mabaya kwa ufufuo wa hukumu. Mimi siwezi kufanya kitu kwa amri yangu; nahukumu kama ninavyosikia, na hukumu yangu ni ya haki; kwa sababu nafanya sio nitakayo mimi, bali atakayo yeye aliyenituma.”

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.

 

Wasiliana Nasi

Dar es Salaam, Tanzania

+255 758 096 383

[email protected]

Tufuatilie

© Mkatoliki Kiganjani. Haki Zote Zimehifadhiwa.